Jumanne, 20 Oktoba 2015

UMASKINI WA MALI AU UMASKINI WA FIKRA?

Inashangaza kuona watu wanambiwa na kupewa ahadi kuwa wataondolewa umaskini na kuwafanya wawe na maisha mazuri. Umaskini wanaouongelea waheshimiwa ni umaskini upi?kuna umaskini wa fikra, umaskini wa njaa, umaskini wa hela, na umaskini wa elimu,sasa waheshimiwa wakisimama kuwapigia watu tarumbeta ya kuleta mabadiliko na kuondoa umaskini mbona hawaelezei namna na jinsi watakavyo mfanya kila mtanzania aondokane na umaskini wa aina zote zilizotajwa hapo juu?inawezekana ukawafanya watu wote nchi hii wakawa kweli matajiri au ni siasa inayosukuma hayo mambo kuliko utawala wa akili na kufikiri juu ya hao waheshimiwa wayasemayo?Hata nchi zilizoendelea bado zina maskini,inakuwaje sisi Leo tuambiwe kuwa baada ya uchaguzi tunakuwa matajiri bila hata ya kuonyeshwa ishara halisi kimatendo ila kwa maneno ndo kwingi?Hayo yote ni kuongelea mdomoni kuliko kongelea akilini.

UMRI WA UZEE NA MAHITAJI YAKE

Mtu akifikia umri wa uzee anakuwa kama mtoto mdogo. Usione daima mzee anakusumbua na kukuambia mambo ambayo unayaona ni ya kitoto, Bali ndo asili ya binadamu.Ukiona hivyo msikilize kwa makini Huyo mzee awe Baba au Mama na mpe analohitaji maana na yeye alikuwa kijana kama wewe na hakuomba awe mzee ila ni kwa sababu ya asili ya binadamu kuwa hivyo.Na wewe pia utafika wakati utakuwa kama huyo mzee.Endelea kushukuru Mungu kwa zawadi ya hao wazazi wazee, usiwaone kama msalaba Bali waone kama msalaba unaopendwa na wenye kubebeka.Maisha ni kubadilishana,ulipokuwa mtoto wao walikuwa vijana wakakutafutia mahitaji namalezi mazuri na wewe pia kama kijana watengenezee wazee wako mahitaji mazuri pindi wanapozeeka na kuonyesha hali ya utoto

ELIMU NA UMUHIMU WAKE

Elimu ya uraia(zamani Siasa) na somo la filosofia ya siasa ni vitu mbavyo katika mapana yake katika nchi yetu havijapewa kipau mbele sana na huwa vinachukuliwa kama masomo ya ziada au nyongeza. Ukosefu wa uhelewa mpana wa mfumo wa siasa na utawala na matabaka yaliyo katika mfumo wa utawala umetufanya wengi tuwabebe walafi na wanyonyaji waliojikita tayari nyuma ya pazia la siasa wakijenga mahekalu.Tukumbuke kuwa mifumo yote tuliyonayo ya utawala haipo kwa ajili ya kumnufaisha mwananchi mwenye kipato duni Bali kujishibisha na kile kinachobaki baada ya kujishibisha kinatupwa kwenye mashimo marefu ambayo hata mlalahoi hawezi weka mkono na kukifikia(utoroshwaji WA hela za walalahoi na kufichwa nje ya nchi-Uswiz).Hao hao ndo wakishashiba wakaona uchaguzi unakaribia ndo hutumia masalia yaliyokuwa yamefichwa ngambo,hela ya haohao walalahoi waliyoisha sahau kama ni hela na jasho lao kuwalaghai wawapigie kula,hela hiyo ndo inatumika kuwanunulia hao walalahoi tishert na kofia ikiwemo kilauri ya pombe na hatimaye humpigia makofi mlafi na kuendelea kumweka madarakani;na kumfanya aendelee kuneemeka kwa kuwaibia zaidi.Maisha bora kwa kila mtanzania yanakujaje?maisha bora kwa kila mtanzania ni kuwajengea watu shule za kata sisizo na miundo mbinu bora za kufanya kazi ikiwemo walimu wa kutosha, maisha bora kwa kila mtanzania ni kuwanyima baadhi ya wahitimu mikopo ya kusoma elimu yajuu wakati huohuo wale wasemao maisha bora kwa kila mtanzania watoto wao hakuna hata mmoja wao aneyesoma shule ya Kata.Au maisha bora kwa kila mtanzania ni kuona watu wanakosa huduma katika hospital za serikali hadi wanapoteza maisha wakati wale walioshikilia ile keki ya juu wakiumwa mafua wanaenda kuyatibu hayo mafua London.Hayo ndo maisha bora kwa kila mtanzania. Timefikia wakati wa kukabidhi mbuzi wetu fisi akatuchungie.Tumefika wakati wa kuchezewa viini macho na kutoa dhamana ya nchi kupitia chezo mazingaombwe unaofahamika kwa wachache ambao 

JIBADILISHE KABLA HUJABADIRISHWA

Itawezekana kupata mabadiliko ikiwa wanaodai hayo mabadiliko hata wao wenyewe hawajajiletea mabadiliko hata kwa mambo madogo waliyonayo?mfano kama mtu anadai mabadiliko wakati hata magugu yaliyozunguka nyumba yake yanamshinda kuyangoa, mtu akishindwa kufagia nyumba yake na kuipanga vizuri na hata akashindwa kupanga chumba chake anapolala mwenyewe sasa ukisikia huyo anadai mabadiliko huyo kweli anadai mabadiliko kutoka ndani ya moyo wake au ni msukumo wa mikumbo ili mradi siku imeenda?Itawezekana kweli kudai mabadiliko ihali mdai mabadiliko hajajibadilisha na kubadilika na hatimaye kudai ili abadilishwe zaidi.Kamwe haitowezekana mabadiliko kwa watu kama watu wenyewe hawajajibadilisha katika vitu vifuatavyo:1.Kujibadilisha kifkra 2.Kujibadilisha kimtizamo hasa juu ya kufikiri,kutenda, na kuchukulia uhalisia wa mambo.3.Kujenga mtizamo chanya na kujikubali mapungufu 4.Kuondoa dhana ya kujihisi wanyonge daima na hivyo kujenga dhana ya kuwa wategemezi daima. Kwa hili ni kuwa dhana ya kutegemea kila kitu kupewa ndo wengi tumejikuta tunaitwa mbumbumbu na hivyo kutengeneza mwanya kwa waheshimiwa kutoa ahadi hewa za mabadiliko yasiyokuwepo.Tusipojibadili namna ya kuchukulia na kufanya mambo tutajikuta hatuna mabadiliko kamwe.Haiwezekani ukalala bila ya kufanya lolote na hapo ukategemea mabadiliko yatokee.Kuleta mabadiliko ni moja ya mapinduzi katika historia.Tukumbuke kuwa hustoria ni kwa wale tu waitengenezayo(history is only for those who make it,never sleep and expect history to be made for you).Mabadiliko yatakuja pale ambapo tulisha anza sisi wenyewe kwa Yale madogo tuliyoanzisha kwa juhudi zetu wenyewe

LUGHA NA MATUMIZI YAKE

Matumizi ya lugha isivyo hitajika yaweza kupoteza ukweli wa mambo kihalisia na kufanya hata watu wasiohusika hata vitu visivyoweza kutumia ufahamu(reasoning) kuonekana kuwa vina hatia. Mara nyingi tumeshuhudia mfano ajali nyingi hapa kwetu na duniani kote.Ajali kama hizo zimehusisha watu kupoteza maisha kutokana na hizo ajali. Mfano tumeshuhudia ajali za vyombo vya moto kama vile pikipiki na magari, ndege,na vinginevyo. Jambo ambalo huwa daima linanishangazaga ni kwenye mawasiliano wakati wa kutoa taarifa baada ya kutokea ajali mfano utasikia mtu anaongea kuwa " nimeangushwa na pikipiki,au nimeangushwa na gari" hivi kweli hii inawezekana kimaongezi kuwa mtu ameangushwa na pikipiki au gari? mimi naona kuwa hiyo siyo sahihi kamwe.Daima mtu huwa ndo anaiangusha pikipiki au gari maana hivi vifaa vya usafiri huwa havina akili au utashi wa kuamua kumdondosha mtu bali uzembe wa mtu huwa ndo unamfanya adondoshwe au aangushwe na hicho kifaa cha usafiri.Hiyo ndo kawaida yetu binadamu kuwa huwa hatupendi kuwajibika kutokana na uzembe wetu baadala yake ni kuhamishia maumivu na hisia kwa watu na hata vitu visivyo na uhai kuhusika na mikosi tuipatayo. Nimesikia mara nyingi mtu mmoja akisema kuwa kamwe hatopanda pikipiki, nilipomuuliza sababu ya kusema vile akaniambia kuwa ni kwa kuwa pikipiki zimeangusha na kuua watu wengi;swali langu kwake lilibaki kuwa " je pikipiki huwa inaangusha mtu au mtu huwa ndo anaiangusha?" Uwajibikaji ni muhimu kabla ya kuelekeza tuhuma kwa wengine.

KWA NINI WALIMU WANAPATA UJIRA WA KUBABAISHA?

Tujiulize swali la msingi kuwa kama walimu wetu wangelikuwa wanalipwa posho kama za wabunge kwa mwezi kungelitokea nini katika sekta ya elimu?Hivi huyu anayeenda kuwakilisha wananchi katika chombo cha dola ambacho ni moja ya mihili mikuu ya serikali kimaarifa au kielimu huyu inasemwa kuwa walau awe na elimu ya kidato cha nne na zaidi ajue kusoma na kuandika basi. Cha kushangaza na kuchekesha ni kuwa huyu ambaye anasemwa kuwa ajue kusoma na kuandika mara nyingi huwa tunawaona kupitia Luninga wakiwa wamechapa usingizi na kusahau kile kilichowafanya wawe hapo;kisa ni kujua kusoma na kuandika na mwishowe huyo anapata posho Mara nne au tano ya mwalimu au mtu yeyote mtaaluma ambaye kila siku lazima asumbue kichwa chake kufanya kazi Fulani,wakati waheshimiwa wanalala na posho inaingia.Hivi ninani ambaye hawezi simama pale bungeni na kutoa hoja? kusimama pale kunahitaji kuumiza vichwa kweli?jibu ni hapana ila kukaa pale ni sawa na kusema kama waswahili wa mtaani wasemavyo"kula kuku kwa mrija." Hii itakuwa sahihi nikisema kuwa baadhi ya wataaluma wetu hasa maprofessa wetu wa vyuo vikuu wanaacha fani zao na kukimbilia kwenye siasa maana huko kuna ulaji kwa njia ya mtelemko bila ya kusumbua vichwa.Hivi kama hao wanaokimbia fani zao na kuingia katika siasa wangelikuwa wanapewa keki wanayopewa hawa waheshimiwa bungeni tungelikuwa hatua ya juu sana kielimu. Uwezo wa kujenga hoja na fikra hautegemei kusoma na kuandika,Bali unahitaji pia nguvu ya kufikiria na kujenga hoja makini.Wale waliopaswa kushauri wanaoongoza pia nao wanataka kuongoza,je hapo nani atatoa maoni na ushauri kwa wanaoongoza?matokeo yake ni kuishia katika ushabiki usiojenga

MAADILI JUU YA AHADI.

Ahadi yaweza kuleta matumaini ya kuishi kwa muda mrefu bila ya kuona ukweli wenyewe au uhalisia wa hiyo ahadi.Kwa kifupi naweza sema ahadi siyo tofauti na ndoto maana hivyo vyote ni ishara zinazolenga kwenye uhalisia japo zenyewe siyo uhalisia(reality)kamwe. Ahadi ni kama vile mtu kusikia harufu ya chakula kikipikwa au kukaangwa akasikia kushiba kumbe ihali bado ana njaa ya kutosha. Sasa wengi wetu ndo hali tuliyoifikia wakati tukielekea uchaguzi mkuu.Hivi hizi ahadi zinazotolewa na waheshimiwa tukapiga makofi kwa nguvu tukafanana na waliokwisha kula na kushiba, hivi huu ni ukweli na uhalisia au bado tuko kwenye ndoto?.Kuna namna nyingi zakudanganywa na ukakubali kiulaini bila ya manunguniko.Njia mojawapo ni ahadi ambazo ni nusu ya uhalisia na nusu uongo.

KWA NINI KUTAWALIWA NA HISIA BAADALA YA KUTAWALIWA NA UFAHAMU?

Ni jambo la kushangaza kuona watu wanatawaliwa na hisia(feelings) za wengine na kuzifanya hisia zao.Kimsingi kundi la watu wa namna hiyo linakuwa limepoteza malengo na mwelekeo kwa ujumla katika maisha.Ukiangalia ushabiki unaofanywa kwa sasa katika vyama vya siasa unaweza tambua kuwa sio mashabiki wote wanajua walitendalo ila wengi wao huenda kwa mkumbo wa kwa kuwa Fulani kashabikia hebu na Mimi nishabikie kitu ambacho ni hatari katika maendeleo na utu wa kila mmoja wetu.Hivyo hatuko mbali kusema kuwa ushabiki ninamna ya watu kuishi maisha ya wengine ili mradi siku ipite.Ushabiki lazima uwe na tija na malengo pia ya kumnufaisha mwananchi kuliko kumnufaisha mgombea.Ni heri kutoshabikia yale tusiyoyajua maana wanaofaidika ni wengine.Kwa jina la ushabiki wengine wameshanunuliwa kwa kilauri/kiloba wakiwa wamesahau kuwa wanauza utu wao na haki zao kwa vitu vya mpito visivyokumbukwa daima.

NANI AHUDUMIWE NA NANI ALALAMIKIWE?

Kama wanaohudumiwa wanawalaumu na kuwalalamikia sana wanaowahudumia, je wanaohudumia watahudumiwa na nani?na wakilalamikiwa nawao watamlalamikia nani? Siyo vema kulaumu na kulalamika kilawakati maana na hao wanaolalamikiwa wana haki ya kulalamika nao ni binadamu kama binadamu wengine.

MIFUMO NA MADHARA YAKE

Kuna wengi ambao kiutendaji huonekana wema.Tatizo linakuja pale ambapo utendaji wao unazoroteshwa na kumezwa na mfumo mama uliowalea hadi wakaota vitambi na mvi.Hao watendaji daima huishia kuumia na kuzikana nafsi zao ili waendelee kulea na kubeza mifumo iliyowalea hata kama wanaona kuna mapungufu.Wakijaribu kuinua na kupaza sauti zao wanajikuta wanalaumiwa na kulumbambana na hao wazazi wao(mifumo)iliyowalea.Mifumo ipo na inaendelea kuwepo katika jamii ili iendelee kuneemeka.Waendao tofauti na mifumo hao ndo wanaonekana kukimbilia upande mwingine wa shilingi. Pia ikumbukwe kuwa mifumo imetawala nyanja mbalimbali mbali katika jamii yetu. Wale ambao wanaonekana wema na watakatifu na wanaopaza sauti zao wakilalamikia mifumo iliyopo kwa sasa, wakishapewa nyenzo tutashuhudia mda si mrefu wao watajenga mifumo ya namna gani?either mfumo wa kujifaidisha wenyewe au mfumo kwa ajili ya manufaa ya wote?lazima tutambue kuwa binadamu ni fumbo ambalo halijafumbuliwa na lisilo rahisi kueleweka kwa kila mtu.Yule anayelia na kuwafanya wengine walie,je wale waliao wakimfikisha mliaji anapotaka je wao wakianza kulia atawasindikiza na kuwafikisha wanapotaka(wananchi)?Wanaoonekana kuomboleza wakisha fikishwa mahala pao wanapotaka daima hujenga kuta ili kuwazuia waombolezaji wasiingie pale walipofika(Ikulu).Tusikumbwe daima na mikumbo ya kutekwa na kuwa watumwa wa mifumo tusiyo ijua malengo yake.

UCHAGUZI MKUU UMETUFIKIRISHA NINI?

Tunavyokaribia kufanya uchaguzi mkuu baadhi ya mambo yanajitokeza ambapo kabla ya hapo mambo hayo yalikuwa hayajajitokeza japo yalikuwepo kiukimyakimya.Mfano ahadi lukuki zilikuwa hazizungumziki na hao waheshimiwa, kwa kipindi hiki cha uchaguzi ni kipindi ambapo wapiga ramli wanavuna vya kutosha.Nikipindi ambapo ikiwezekana wachawi watagundulika.Tukiendelea zaidi tunaona kuwa kila mmoja anamlaumu mwingine kwa kutokutimiza wajibu wake.Hivi katika kulaumiana ninani alaumiwe?yule aliyepewa dhamana na chama chake awe mtendaji wa serikali au chama chenyewe?Imezoeleka kusikika chama Fulani kinalaumiwa kwa utendaji,je ni halali kulaumu chama au watendaji wake?Maana kikilaumiwa chama maana yake ni kuwa wanalaumiwa wanachama wote kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa kwa ujumla wake, kuna uhalali gani wa kumlaumu mwanachama asiyejua nini linatendeka na ni mipango gani inaendelea kwenye chama chake? Kwa msingi huo tunaona wengi wa wapiga campaign wakiwania ile keki nzito hutumia nafasi hiyo kulaumu chama na wanachamawake wote baadala ya kuelekeza tuhuma kwa watendaji.Mbegu hiyo hupandikizwa kwa watu nao watu huamini kuwa chama ni kibaya.Huo ni mchezo wa siasa ambao hutumika kuwafanya wananchi waamini visivyo.Mchezo wa siasa ni mchezo daima ambao wengi huuita kuchafuana(mchezo mchafu).Hivyo kuchafuana katika siasa huwa kunajumisha kuwachafua wote bila ya kuangalia ninani mhusika zaidi ya wote katika kundi.Katika lugha na maongezi ya kifalsafa na lugha ya kifalsafa kuongea kwa ufahamu wa namna hiyo(reasoning) huitwa "Fallacy of generalization),yaani kuacha kuongelea jambo husika au mhusika na baadala yake wanashambuliwa hata wasiohusika kamwe.

MCHEZO WA SIASA NI MCHEZO WA NAMNA GANI?

Tunavyokaribia kufanya uchaguzi mkuu baadhi ya mambo yanajitokeza ambapo kabla ya hapo mambo hayo yalikuwa hayajajitokeza japo yalikuwepo kiukimyakimya.Mfano ahadi lukuki zilikuwa hazizungumziki na hao waheshimiwa, kwa kipindi hiki cha uchaguzi ni kipindi ambapo wapiga ramli wanavuna vya kutosha.Nikipindi ambapo ikiwezekana wachawi watagundulika.Tukiendelea zaidi tunaona kuwa kila mmoja anamlaumu mwingine kwa kutokutimiza wajibu wake.Hivi katika kulaumiana ninani alaumiwe?yule aliyepewa dhamana na chama chake awe mtendaji wa serikali au chama chenyewe?Imezoeleka kusikika chama Fulani kinalaumiwa kwa utendaji,je ni halali kulaumu chama au watendaji wake?Maana kikilaumiwa chama maana yake ni kuwa wanalaumiwa wanachama wote kuanzia ngazi ya kitongoji hadi taifa kwa ujumla wake, kuna uhalali gani wa kumlaumu mwanachama asiyejua nini linatendeka na ni mipango gani inaendelea kwenye chama chake? Kwa msingi huo tunaona wengi wa wapiga campaign wakiwania ile keki nzito hutumia nafasi hiyo kulaumu chama na wanachamawake wote baadala ya kuelekeza tuhuma kwa watendaji.Mbegu hiyo hupandikizwa kwa watu nao watu huamini kuwa chama ni kibaya.Huo ni mchezo wa siasa ambao hutumika kuwafanya wananchi waamini visivyo.Mchezo wa siasa ni mchezo daima ambao wengi huuita kuchafuana(mchezo mchafu).Hivyo kuchafuana katika siasa huwa kunajumisha kuwachafua wote bila ya kuangalia ninani mhusika zaidi ya wote katika kundi.Katika lugha na maongezi ya kifalsafa na lugha ya kifalsafa kuongea kwa ufahamu wa namna hiyo(reasoning) huitwa "Fallacy of generalization),yaani kuacha kuongelea jambo husika au mhusika na baadala yake wanashambuliwa hata wasiohusika kamwe.

HUU NI WENDAWAZIMU KUPIGA BARABARA DEKI AU?

Nijambo la kutafakarisha kuona watu wanapiga barabara deki tena kwa nguvu zote! na hili kimsingi siyo jambo la kawaida hata kidogo.Waweza jiuliza nini kinawasukuma watu kufanya hivyo?je wanafanya hivyo kwa ushabiki au kufanya hivyo kunaashiria jambo Fulani? Kama tujuavyo watu wakifanya hivyo wanakuwa wanaashiria jambo fulani kwa kutarajia litokee na kuwafanya wawe katika hali fulani ya maisha. Tunajua kabisa kuwa alama zionyeshapo uendapo huwa daima zinasaidia kuonyesha mahali sahihi unapohitaji kwenda japo alama zenyewe siyo mahali unapotaka kwenda. Tukiona watu wanapiga deki na kupangusa Barabara wanakuwa hasa wanatoa ishara gani? hapo twaweza kuwa na majibu na fikra nyingi. Mojawapo ikiwa ni kwamba wamechoshwa na mfumo mbovu wa uongozi wanataka uongozi mpya na dira mpya ya maendeleo, au kwamba wananchi wanataka sasa kupumulia mahala pazuri pasipo hila wala uyanganyi wala ufisadi n.k hayo ni baadhi ya majibu waliyonayo wapiga kura.Kiuhalisia siyo jambo la kufikirika watu kutumia mda wao mwingi kusafisha barabara pasipo kuambiwa kufanya hivyo au pasipo malipo isipokuwa kuna jambo fulani ambalo kwa wasio funguka macho bado ni kitendawili.

MTU NA UTU WAKE

Ukitaka kutambua utu wa mtu na kumjua yeye ninani mpe Uhuru wa umfanyie nini?hapo ni dhahiri kuwa utapata majibu mengi kutoka kwa huyo mtu juu ya analotaka umfanyie hata kama mengine yapo juu ya uwezo wake.Katika nafasi hiyo utapata kutambua kama huyo mtu ni mchoyo na pia mwenye uchu wa kutaka kutawala au pia utapata kujua unyenyekevu wa huyo mtu kadiri ya kitu ambacho amekuomba ukamfanyie.Sasa tuje ngambo nyingine ya Shilingi ambapo Leo hii tumeshuhudia wale waliokuja kutuomba dhamana ya kuongoza nchi.Wao wakati wanahangaika ili tuwape dhamana ya kutuongoza mambo yamekuwa kama ifuatavyo:1.Wao wamekuja na bado wanazidi kuja kwetu na tumewauliza "je mwataka tuwafanyie nini?" Wao wakajibu kwa sauti kubwa "mtupigie kura ya ndiyo katika uchaguzi mkuu ujao."2.Pindi na sisi ilipokuwa zamu yetu juu ya wao watufanyie nini, wamekuja na majibu mbalimbali yenye kutia moyo japo hayana uhakika asilimia mia moja.Moja ya majibu mepesimepesi ni kufuta baadhi ya Kodi, Elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.Kuanzisha viwanda, kuhakikisha kuwa vijana wote(waliosoma na wasiosoma)wanapata ajira na wanakuwa na maisha mazuri n.k.Hayo yote ni mazuri sana ila wengi wetu tunasahau kuwa siyo kila ahadi utekelezeka! Kwa Mawazo yangu ni kuwa itakuwa rahisi kwetu kutoa majibu ya maswali yetu ya tuwafanyie nini waheshimiwa maana majibu yanaeleweka, kuwa tutawapigia kura ya ndiyo.Wasiwasi unakuja kwa majibu ya maswali yetu kwao kuwa watatufanyia nini?majibu yao kwetu yamekuja na ahadi ambazo ni vigumu kuamini kuwa zitatekelezeka.Tunasahau kuwa Siasa ni mchezo ambao siyo wote twaweza kuucheza. Punde tutashuhudia kama tulidanganywa juu ya hizo ahadi au la! wakishapewa hayo majukumu ndoo itakuwa kutekeleza au kutokuteleza hizo ahadi.Hofu yangu ni kwamba kwa nchi kama Tanzania,Ahadi zilizotolewa baadhi ziko nje ya uwezo wake, kama vile Elimu bure na ajira kwa kila mtanzania hasa vijana.Hayo yote ni majibu ya tutafanyiwa nini.Yatubidi tufunguke macho na kuelewa kati ya kuambiwa ukweli au kulaghaiwa.

LUGHA YA BAO LA MKONO

Kwa sasa tunaambiwa lugha ya bao la mkono! bao la mkono halikulezewa vizuri na kuzungumzika vizuri.Mtoa hoja angelielezea vizuri ni mchezo gani ambapo bao la mkono ni marufuku mfano katika kucheza mpira wa miguu ukifunga bao la mkono jua kuwa kuna adhabu juu yake(Penalty) wakati kama unacheza Mpira wa mikono(volleyball au Basketball) gori la mkono hapo hapo halina shida. Shida ni pale bao la mkono linafungwa wakati wa mchezo wa mpira wa kutumia miguu.Afungaye kutumia mkono kwa mchezo wa Mpira wa miguu hapo inamhitaji abadilike. Katika mfumo wetu wa utawala yaonekana wananchi wameumizwa vibaya na kufikiria vinginevyo kwamba mabao yanayofungwa siyo halali kwa kuwa mchezo unaochezwa ni mchezo wa mpira wa miguu lakini bado mabao yanayofungwa ni ya mkono pasipo halali(utumiaji wa nguvu kupita kiasi na rushwa).Bao la mkono litatambulika kuwa hivyo na halali pindi mchezo ukiwa wa kuchezwa kwa mikono na siyo miguu.Kama wananchi wanalalamikia bao la mkono hii inamaana gani? kwamba mchezo unaochezwa ni wa miguu ambao kiutaratibu lazima bao kama bao linafungwa kwa miguu,Ila matokeo yake washangiliaji wanaona bao linafungwa kwa mkono wanashangaa na kufikiri kutowezekana kwa hilo bao lililofungwa na wakati huo refaree anaweka tiki kuwa ni bao stahiki mbali ya kujuakuwa siyo halali.Tujiulize kuwa katika uwanja wa Siasa wachezaji wanacheza mchezo gani? wa kukubali mshindi halali au lile bao la mkono?